7 Mei 2025 - 17:21
Ayatollah Khamenei: Jukumu la (Hawza) Chuo cha Kidini ni Kuchora Mipaka Mikuu na Midogo ya Ustaarabu mpya wa Kiislamu

"Kazi kuu na ya msingi ya Hawza ni (البَلاغُ المُبین‌) kufikisha ujumbe wa dini kwa uwazi na ufasaha (ubalighi wa wazi - Kwa maana: Kufikisha ujumbe kwa uwazi na uthabiti na kwa namna ambayo haiachi shaka yoyote -). Miongoni mwa vielelezo vyake muhimu kabisa ni kuchora na kueleza kwa uwazi mistari (mipaka) mikuu na ya kando ( au midogo) ya ustaarabu mpya wa Kiislamu, pamoja na kuifafanua, kuieneza, na kuikuza katika jamii kama sehemu ya utamaduni."

 Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Kimataifa la AhlulBayt (as) – ABNA – Ayatollah al-Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe wake kwa kongamano la kimataifa la kuadhimisha miaka 100 ya kuanzishwa upya kwa Hawza ya Kielimu ya Qom, alielezea vipengele na majukumu mbalimbali ya Hawza, na akazungumzia masharti ya kufanikisha "Hawza iliyo mstari wa mbele na ambayo ni kielelezo bora."

Hawza hiyo inapaswa kuwa na sifa za ubunifu, ukuaji wa kielimu, ufuatiliaji wa masuala ya kisasa, uwezo wa kujibu changamoto mpya, maadili mema, ari ya maendeleo na jihadi, pamoja na kuwa na utambulisho wa kimapinduzi. Pia inapaswa kuwa na uwezo wa kubuni mifumo ya uendeshaji wa jamii.

Kiongozi wa Mapinduzi alisisitiza kuwa jukumu kuu la Hawza ni "ubalighi wa wazi" (بلاغ مبین), yaani kufikisha ujumbe wa dini kwa namna ambayo haiachi nafasi ya shaka. Miongoni mwa mifano bora ya jukumu hili ni kuchora kwa uwazi mistari mikuu na midogo ya ustaarabu mpya wa Kiislamu, pamoja na kuufafanua, kuueneza na kuukuza katika jamii."

Matini ya ujumbe kamili wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kama ifuatavyo

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote. Rehema na amani ziwe juu ya Bwana wetu Muhammad al-Mustafa na watu wa nyumbani kwake watoharifu, hususan juu ya Baqiyyatullah (Imamu wa Zama) katika walimwengu.

"Kuchomoza kwa Hawza Tukufu ya Qom mwanzoni mwa karne ya kumi na nne ya Hijria (Shamsia), ilikuwa tukio la kipekee lisilo na mfano wake. Tukio hili lilijiri katikati ya matukio makubwa na ya kuumiza, ambayo yalikuwa yameifanya hali ya eneo la Asia ya Magharibi kuwa ya giza totoro, na kuyumbisha maisha ya mataifa yake kwa hali ya machafuko na uharibifu.

Chanzo cha matatizo haya makubwa na ya muda mrefu kilikuwa ni kuingilia kati kwa mataifa ya kikoloni na washindi wa Vita ya Kwanza ya Dunia, waliotumia kila njia ili kutwaa na kutawala maeneo haya nyeti yaliyojaa rasilimali za chini ya ardhi. Kwa kutumia nguvu za kijeshi, mikakati ya kisiasa, hongo, kutumia wasaliti wa ndani, vyombo vya habari na utamaduni, na kila njia waliyoiona kuwa na manufaa, waliweza kutimiza malengo yao.

Nchini Iraq, waliunda Serikali ya kifalme inayotawaliwa kwa niaba yao. Katika eneo la Sham (Syria na Lebanon), Uingereza na Ufaransa waligawana maeneo ya ukoloni kwa kuanzisha mifumo ya kikabila na kuweka familia ya kifalme ya Uingereza madarakani. Walieneza ukandamizaji na mateso dhidi ya watu, hasa Waislamu na wanavyuoni wa dini. Nchini Iran, walimkuza polepole Mkazakhi mkatili - (Mkazakhi maana yake ni mtu ambaye ni mkatili na mwenye tamaa, na ambaye pia hana sifa za utu au heshima ya kibinadamu. Hivyo Neno "قزّاق" Mkazakhi linapotumika linakuwa na maana hiyo inayohusiana na mtu aliye na tabia ya kikatili na mwenye kufanya vitendo vya unyanyasaji) - mwenye ukatili, tamaa, na asiye na utu hadi kuwa Waziri Mkuu na kisha Mfalme. Katika nchi ya Palestina, walianzisha mchakato wa kuhamisha kwa polepole watu wa Kizayuni, kuwapa silaha, na kuandaa mazingira kwa ajili ya kutokeza kwa gonjwa hatari la saratani (kansa) katika moyo wa ulimwengu wa Kiislamu.

Popote palipojitokeza upinzani dhidi ya mipango yao — iwe Iraq, Sham, Palestina au Iran — waliikandamiza kwa ukatili. Katika miji kama Najaf, waliwakamata kwa pamoja wanavyuoni, waliwafukuza kwa udhalilishaji marjaa wakubwa kama Mirza Naeini, Sayyid Abul-Hasan Isfahani na Sheikh Mahdi Khalisi, na walifanya upekuzi nyumba hadi nyumba ili kuwakamata wapiganaji wa jihadi. Mataifa yalizama katika hofu na mkanganyiko, na matumaini yalizimika. Nchini Iran, wapiganaji (wana jihadi) wa Gilan, Tabriz, na Mashhad walimwaga damu zao, huku wasaliti waliokuwa wakishiriki mikataba ya aibu wakiwekwa madarakani.

Ni katika mazingira haya ya giza, na machungu na ya kukata tamaa, ndipo nyota ya Qom ilipochomoza. Kwa mkono wa uweza wa Mwenyezi Mungu, alikuja Faqihi mkubwa, Mchamungu na mzoefu, ambaye alihama kuja Qom na kuhuisha upya hawza iliyokuwa imekufa na kufifia. Alipanda mche mpya na wa baraka katika ardhi hiyo ngumu ya wakati huo, karibu na Haram ya Binti Mtukufu wa Imam Mussa ibn Ja'far (A.S), katika ardhi iliyokuwa tayari kwa ukuaji."

"Qom wakati wa kuwasili kwa Ayatollah Haeri, miongoni mwa wanazuoni wakubwa, haikuwa tupu; wanazuoni wakubwa kama Ayatollah Mirza Muhammad Arbab, Sheikh Abul-Qasim Kabir, na wengine wengi waliishi katika mji huu. Hata hivyo, sanaa kuu ya kuanzisha Hawza ya Kielimu, yaani, shule ya kisayansi, wanazuoni, dini, na uadilifu, kwa ufundi wake wote na mipango yake, ilikuwa ni kazi ya mtu mkubwa kama Ayatollah Haj Sheikh Abdul-Karim Haeri (Allah amuinue daraja yake katika pepo).

Ayatollah Khamenei: Jukumu la (Hawza) Chuo cha Kidini ni Kuchora Mipaka Mikuu na Midogo ya Ustaarabu mpya wa Kiislamu

Ayatollah Haj Sheikh Abdul-Karim Haeri (Allah amuinue daraja yake katika pepo)

Uzoefu wa miaka nane wa kuanzisha na kuongoza Hawza yenye mafanikio huko Arak, pamoja na mazoezi ya karibu na kiongozi mkubwa wa Shia, Mirza Shirazi huko Samarra, na kuona mikakati yake ya kuanzisha na kuongoza Hawza ya mji huo, vilimsaidia kwa njia nzuri; ufanisi wake, ujasiri, motisha na matumaini viliendelea kumtuma mbele katika njia hii ngumu.

Hawza katika miaka ya mwanzo, ilikua kwa juhudi thabiti na za unyenyekevu kutoka kwao, chini ya uongozi wa Ayatollah Haeri, wakati wa serikali ya kidikteta ya Reza Khan, ambaye alikuwa na malengo ya kuharibu alama na misingi ya dini. Alikuwa na nia ya kuondoa kila dalili ya dini kwa kutumia nguvu, lakini alianguka na alimalizika, huku Hawza ikichomoza, ikikua, na kuzaa mapinduzi kama ya Imam Khomeini (R.A).

Hawza hii ilikuwa, miaka kadhaa baada ya kifo cha mwasisi wake, ndio iliyoleta kiongozi mkubwa Ayatollah Borujerdi, ambaye aliifanya kuwa kilele cha kisomi na utangazaji wa Shia katika dunia nzima. Hivyo, Hawza hii ilikuja kuwa chanzo cha nguvu na mafanikio kwa ajili ya mapinduzi ya Kiislamu. Hivyo ndivyo ilivyofanikiwa kuangusha utawala dhalimu wa kifalme wa Iran.Ayatollah Khamenei: Jukumu la (Hawza) Chuo cha Kidini ni Kuchora Mipaka Mikuu na Midogo ya Ustaarabu mpya wa Kiislamu

Ayatollah Khamenei: Jukumu la (Hawza) Chuo cha Kidini ni Kuchora Mipaka Mikuu na Midogo ya Ustaarabu mpya wa Kiislamu

Ayatollah Sayyid Hossein Ali Tabatabaei Borujerdi (R.A)

Wahadhiri wa Hawza hii walienda mbele na kuifanya Iran kuwa mfano wa harakati ya Kiislamu ulimwenguni. Kwa msaada wa uongozi wa kiroho wa Ayatollah Khomeini, damu ilishinda upanga, na kwa juhudi zake, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ulizaliwa. Kwa shujaa na imani, Taifa la Iran lilisimama mbele ya vitisho na likafanikiwa. Leo hii, Iran inendelea kutimiza mafanikio mbalimbali katika maeneo mengi ya maisha kutokana na misingi ya kiongozi huyu (Ayatollah Imam Khomein, Mwenyezi Mungu Amrehemu).

Ayatollah Khamenei: Jukumu la (Hawza) Chuo cha Kidini ni Kuchora Mipaka Mikuu na Midogo ya Ustaarabu mpya wa Kiislamu

Tunamwomba Mwenyezi Mungu ampe rehema na amani mwasisi wa Hawza hii tukufu na yenye baraka, Ayatollah Haj Sheikh Abdul-Karim Haeri.

Sasa, ni muhimu kusema maneno kuhusu baadhi ya masuala ambayo yanaonekana kuwa muhimu kwa mafanikio ya Hawza ya kisasa na ya kesho. Tunatumaini kuwa hili litasaidia katika kuzidi kuipelekea Hawza "mbele na kuwa ya kipekee."

Kwanza, neno "Hawza ya Kielimu" na maana yake ya kina:

Lugha inayotumika kuhusu hili mara nyingi ni fupi na haina uwezo wa kueleza kikamilifu. Hawza, kinyume na kile kinachozungumziwa na lugha hii, si tu taasisi ya kufundisha na kujifunza, bali ni jumla ya elimu, malezi, na kazi za kijamii na kisiasa. Maeneo mbalimbali ya maana ya neno hili yanaweza kufafanuliwa kama ifuatavyo:

1. Kituo cha kielimu chenye utaalamu maalum;
2. Kituo cha kulea watu waliotakasika na wenye ufanisi kwa ajili ya kuongoza jamii kidini na kiakhlaqi;
3. Safu ya mbele katika kukabiliana na vitisho vya maadui katika nyanja mbalimbali;
4. Kituo cha uzalishaji na ufafanuzi wa fikra za Kiislamu kuhusu mifumo ya kijamii—kuanzia mfumo wa kisiasa na muundo wake wa ndani na nje, hadi mifumo ya uendeshaji wa nchi, familia na mahusiano ya kijamii—kwa mujibu wa fiqhi, falsafa, na mfumo wa maadili wa Uislamu;
5. Kituo, na huenda kilele, cha ubunifu wa kiustaarabu na mtazamo wa mbele kwa mustakabali, ndani ya wigo wa ujumbe wa kimataifa wa Uislamu.

Vichwa hivi vya habari ndiyo vinavyoipa maana dhati neno "Hawza ya Kielimu", na vinaonesha vipengele vyake vya ndani au kwa kauli nyingine "matarajio" yanayowekewa taasisi hii. Na ni haya ndiyo kwamba juhudi za kuimarisha na kuendeleza maeneo haya zinaweza kuifanya Hawza kuwa kweli ni yenye "kuendelea na ni ya kipekee", na ikawa na uwezo wa kukabiliana na changamoto na hatari zinazowezekana kutokea.

Kuhusu kila moja ya haya, kuna hali halisi na pia maoni mbalimbali ambayo kwa muhtasari yanaweza kuelezwa namna hii kama ifuatavyo:


Kwanza – Kituo Cha Kielimu:

Hawza ya Qom ni mrithi wa hazina kubwa ya kielimu ya Shia. Hazina hii ya kipekee ni zao la fikra na utafiti wa maelfu ya wanazuoni wa Kiislamu katika elimu kama fiqhi, teolojia (kalaam), falsafa, tafsiri ya Qur'ani na hadithi, katika kipindi cha zaidi ya miaka elfu moja.

Kabla ya ugunduzi wa sayansi za kiasili katika karne za hivi karibuni, Hawza za Shia zilikuwa pia sehemu ya kujifunzia sayansi nyingine. Lakini katika zama zote, mhimili mkuu wa elimu na utafiti katika Hawza umekuwa ni "Fiqhi", na kisha kwa kiwango kidogo zaidi, teolojia, falsafa na hadithi.

Maendeleo ya kielimu katika Fiqhi yanayoonekana kwa wataalamu yamekuwa hatua kwa hatua, kuanzia zama za Sheikh Tusi, kisha zama za Muhakiki Hilli, kisha zama za Shahid, kisha zama za Muhakiki Ardabili, kisha zama za Sheikh Ansari hadi zama za sasa. Kigezo cha maendeleo katika Fiqhi ni kuongezeka kwa maudhui ya kielimu, yaani uundaji wa maarifa mapya na kuboresha kiwango cha elimu.

Lakini katika zama hizi za mabadiliko ya haraka na makubwa ya fikra na vitendo—hasa katika karne hii ya sasa—tunapaswa kuwa na matarajio makubwa zaidi kuhusu maendeleo ya kielimu ya Hawza.

Kuhusu Elimu ya Fiqhi, Mambo Haya Yanastahili Kuzingatiwa:

Kwanza, fiqhi ni jibu la dini kwa mahitaji ya kimatendo ya mtu binafsi na jamii. Kwa sababu ya mabadiliko ya fikra na mantiki ya vizazi vipya, majibu haya leo yanapaswa kuwa na msingi madhubuti wa kielimu na kiakili, na vilevile yawe yanaeleweka kwa urahisi na yanafaa kufuatwa.

Pili, changamoto nyingi mpya na tata katika maisha ya sasa ya watu zimezua maswali yasiyokuwepo hapo kabla, ambayo fiqhi ya kisasa lazima iwe na majibu tayari kwao.

Tatu, kwa kuwa sasa mfumo wa kisiasa wa Kiislamu umeundwa, swali kuu ni mtazamo wa jumla wa Sheria ya Kiislamu kuhusu vipengele vyote vya maisha ya binadamu—kuanzia mtazamo kuhusu mwanadamu na nafasi yake, malengo ya maisha yake, hadi mtazamo kuhusu jamii bora, siasa, mamlaka, uhusiano wa kijamii, familia, jinsia, uadilifu na vipengele vingine vya maisha. Kila Fat'wa ya Faqihi inapaswa kuonyesha sehemu ya mtazamo huu mpana.

Jambo muhimu ili kufikia sifa hizi ni kwamba Faqihi lazima awe na maarifa ya kina kuhusu nyanja zote za elimu ya dini, na pia awe na uelewa wa kutosha wa maarifa ya kisasa ya binadamu, hasa katika fani za sayansi ya jamii na elimu zinazohusiana na maisha ya Mwanadamu.

Ni lazima tukubali kwamba hazina kubwa ya elimu iliyokusanywa katika Hawza ina uwezo wa kumfikisha Mwanafunzi katika kiwango hiki cha kielimu, mradi baadhi ya changamoto katika mfumo wa sasa wa ujifunzaji zitatambuliwa kwa makini na kutatuliwa kwa umahiri.


Baadhi ya changamoto hizo ni kama zifuatazo:

1. Urefu wa muda wa masomo:
Katika mfumo wa sasa, kipindi cha kusoma vitabu vya msingi huwa kirefu mno. Mwanafunzi hulazimika kusoma kitabu kigumu cha mwanazuoni mkubwa kama maandiko ya darasa la juu, ilhali bado yuko kwenye hatua ya awali ya masomo. Vitabu hivi vilitungwa kwa ajili ya kipindi cha utafiti wa kifiqhi (ijtihad), si kwa hatua ya maandalizi. Matokeo yake ni kuchelewesha safari ya kielimu ya Mwanafunzi.

Vitabu vya kufundishia vinapaswa kuandikwa kwa maudhui na lugha inayoendana na kiwango cha awali cha Mwanafunzi.
Juhudi za wanazuoni kama A'khund Khurasani, Ayatollah Haeri na Sayyid Sadruddin Sadr za kubadili vitabu kama Qawanin, Rasa'il  na  Fusul na kutumia badala ya hivyo: Kifayah, Durar al-Fawa'id na Khilasat al-Fusul zilitokana na kutambua umuhimu huu—na hilo ni licha ya kwamba wao waliishi katika zama ambazo wanafunzi hawakuwa wanakabiliwa na changamoto nyingi za kifikra na kijamii kama za leo.

2. Kipaumbele katika masuala ya Fiqhi:
Leo, baada ya kuundwa kwa dola ya Kiislamu na kuanza kwa utawala wa Kiislamu, masuala mapya na muhimu yameibuka ambayo zamani hayakuzingatiwa sana katika fiqhi. Haya ni pamoja na:

  • Mahusiano kati ya Serikali na raia wake, au kati ya Serikali ya Kiislamu na Mataifa mengine;
  • Dhana ya Nafy Sabil (kuzuia ukoloni wa kisheria au kisiasa);
  • Mfumo wa uchumi wa Kiislamu na misingi yake;
  • Chanzo cha mamlaka katika mtazamo wa Kiislamu;
  • Nafasi ya watu katika uongozi;
  • Msimamo wa Kiislamu katika masuala muhimu ya kimataifa na dhidi ya mifumo ya kidhalimu;
  • Maana na yaliyomo ya uadilifu;
  • Na masuala mengine mengi muhimu na ya msingi ambayo yanahitaji majibu ya kifiqhi kwa ajili ya sasa na kesho ya nchi.

Baadhi ya masuala haya pia yana sura ya kiitikadi (kalaam), ambayo inapaswa kujadiliwa katika nafasi yake maalum.

Katika mfumo wa sasa wa kazi wa Hawza, haswa upande wa fiqhi, hakuna uangalifu wa kutosha kwa masuala haya ya kipaumbele. Wakati mwingine, baadhi ya ujuzi wa kifikra ambao unapaswa kuwa ni chombo cha kusaidia kuelekea hukumu ya kisheria au baadhi ya masuala ya fiqhi yasiyo ya kipaumbele, humvutia Faqihi au mtafiti kwa namna ya kusisimua kiasi kwamba humpeleka mbali na masuala ya msingi na ya dharura. Hii hupelekea kupoteza fursa zisizoweza kurejeshwa, pamoja na rasilimali za watu na fedha, bila kusaidia chochote katika kueleza mfumo wa maisha ya Kiislamu au kuongoza jamii katika kipindi cha mashambulizi ya kifikra ya ukafiri.

Ikiwa lengo la kazi ya kielimu ni kuonyesha umaarufu wa kielimu au kushindana katika kujionesha kuwa mwanazuoni, basi hiyo ni mfano wa matendo ya kidunia yasiyo na thamani ya kiroho, na ni mfano wa aliyefanya matamanio yake kuwa mungu wake kama ilivyosemwa: «اِتَّخَذَ إِلٰهَهُ هَوَاه» — "Ameyafanya matamanio yake kuwa mungu wake." (Surat Al-Jathiyah: 23).

 Pili – Malezi ya Watu Waliotakasika na Wenye Ufanisi:

Hawza (chuo cha kidini) ni taasisi ya kuelekea nje ya mipaka yake. Matokeo ya elimu kutoka hawza, katika ngazi zote, ni kwa ajili ya kuhudumia fikra na utamaduni wa jamii na wanadamu. Hawza ina wajibu wa “tabligh mubiin” — yaani kuwasilisha ujumbe wa dini kwa uwazi kamili. Upana wa tabligh hii ni mkubwa mno: kutoka mafundisho ya juu ya tauhidi hadi wajibu wa mtu binafsi wa kidini; kutoka kufafanua mfumo wa Kiislamu na muundo wake hadi mtindo wa maisha, mazingira, ulinzi wa asili na hata haki za wanyama, pamoja na maeneo mengine mengi ya maisha ya mwanadamu.

Hawza za kielimu tangu zamani zimelibeba jukumu hili zito, na wahitimu wake wengi wamejikita katika ulinganiaji wa dini kwa njia mbalimbali. Baada ya Mapinduzi ya Kiislamu, taasisi zilianzishwa ili kusaidia kupanga na kuimarisha juhudi hizi za tabligh ndani ya hawza. Huduma zao na za wengine wanaojihusisha na kazi ya tabligh hazipaswi kupuuzwa.

Hata hivyo, kilicho muhimu ni kufahamu hali halisi ya fikra na tamaduni za jamii, na kuleta uwiano kati ya kile kinachofundishwa na ukweli wa maisha ya watu — hasa vijana. Katika eneo hili, hawza ina udhaifu. Mamia ya makala, majarida, mihadhara ya majlisi na redio/televisheni haziwezi kupambana ipasavyo na wimbi la propaganda zenye udanganyifu na kushughulikia kikamilifu wajibu wa tabligh mubiin.


Vipengele Viwili Muhimu Vinavyokosekana Hawzani: Elimu na Malezi ya Kiakhlaki

Kufikisha ujumbe ulio wa kisasa, unaojibu changamoto za sasa, na unaotimiza lengo la dini, kunahitaji elimu mahsusi.
Lazima pawepo na mfumo wa kielimu unaomfundisha Mwanafunzi mbinu za kuzungumza, namna ya kushawishi, kuelewa mitazamo ya jamii na vyombo vya habari (pamoja na mitandao ya kijamii), na jinsi ya kushughulika kwa nidhamu na wale wanaopinga au wanaoleta hoja kinyume. Kupitia mazoezi ya vitendo katika muda mfupi, Mwanafunzi awe tayari kuingia katika uwanja huo.

Pia ni muhimu sana kukusanya hoja na propaganda mpya zenye madhara ya kiakili na kimaadili, kisha kuandaa majibu makali, yanayoeleweke vizuri na yanayofaa katika lugha ya kizazi cha sasa. Kwa wakati huo huo, lazima maandalizi ya kielimu kuhusu maarifa muhimu ya dini yalingane na hali ya fikra na tamaduni ya vijana, wanafunzi na familia, katika mfumo wa kifurushi cha elimu. Hii ndiyo "elimu" inayohitajika katika sehemu hii ya tabligh.


Tabligh Inahitaji Kushambulia Fikra Potofu, Si tu Kujibu Hoja

Katika ulinganiaji, msimamo wa kuwasilisha hoja chanya (hata ya kukosoa) ni muhimu zaidi kuliko kujilinda tu dhidi ya hoja pinzani. Licha ya umuhimu wa kupinga mashaka na hoja potofu, mfumo wa tabligh usiwe tu wa kujibu hoja, bali unapaswa pia kukosoa misingi ya tamaduni potofu za kimagharibi ambazo zinaendelea kuporomoka kwa kasi. Hawza inayozalisha wanafalsafa na wanateolojia haipaswi tu kujibu mashaka, bali ianzishe mijadala mikali inayowalazimisha wapotoshaji kujibu.

Kuanzisha mfumo huu wa elimu ya tabligh ni miongoni mwa vipaumbele vya Hawza. Hii ni njia ya kulea "Mwanamapambano wa Kitamaduni", na kwa kuzingatia kwamba maadui wa dini kwa dhati wanalea majeshi yao hasa katika maeneo nyeti, basi kazi hii inahitaji kuchukuliwa kwa uzito na kwa kasi.


Malezi ya Kiakhlaki - Tabia Njema - (Tahdhib)

Malezi ya kiakhlaki si kufundisha kuwa mtulivu tu au kujitenga.
Sehemu kubwa ya kazi ya Mwanamapambano wa kitamaduni ni kuwalingania watu kwenye ucha-Mungu na tabia njema. Lakini, kama mwalimu hana sifa hizi mwenyewe, basi mawaidha yake hayatakuwa na athari wala baraka. Hawza inahitaji jitihada zaidi kuliko zamani katika kusisitiza mafunzo ya akhlaqi.

Enyi wanafunzi wa Hawza — kwa sababu ya nyoyo zenu safi na ndimi za ukweli — hakika mnaweza kuwalea vijana wa kizazi hiki kiakhlaki, mradi muanze kwanza na nafsi zenu.
Ikhlasi (unyofu wa nia), na kuachana na tamaa ya mali, sifa, au madaraka, ndizo funguo za kuingia kwenye dunia ya kiroho na ukweli.
Hapo ndipo kazi ngumu ya tabligh itageuka kuwa ladha na yenye athari kubwa. Taabu za maisha ya mwanafunzi wa hawza, badala ya kuwa kizuizi, zitakuwa chachu ya kudumu kwa azimio na nia madhubuti.


Nasihi: Kamwe usiangalie uwanja wa tabligh kama uwanja usio na washindani. Usikose hata kwa muda mfupi kukabiliana na mashaka na propaganda mpya zinazozuka kila mara.

Katika sehemu hii ya kazi ya malezi, pamoja na kulea watu kwa ajili ya Bala'ghu mubiin - au -  (Tabligh ya Wazi), inapaswa pia kuwa na mpango wa kulea watu kwa ajili ya kazi maalum za mfumo wa Kiislamu, kwa ajili ya uendeshaji wa serikali, na pia kwa ajili ya kusimamia mambo ya ndani ya Hawza yenyewe — mambo ambayo yanahitaji mjadala tofauti.

 Sehemu ya Tatu – Mstari wa Mbele wa Mapambano Dhidi ya Vitisho vya Adui katika Nyanja Mbalimbali

Hii ni moja kati ya sura zisizojulikana sana za hawza za kielimu za Kiislamu na mchango wa jumla wa maulamaa wa dini. Bila shaka, hakuna harakati yoyote ya mabadiliko au mapinduzi katika kipindi cha miaka 150 iliyopita huko Iran na Iraq ambayo haikuongozwa au kushirikiwa kwa karibu na wanazuoni wa dini. Hili ni jambo linalodhihirisha kwa wazi asili ya kipekee ya taasisi za elimu ya dini (hawza).

Katika kipindi hicho chote, kila mara kulipotokea juhudi za ukoloni na udikteta kutaka kutawala, ni wanazuoni wa dini peke yao waliotangulia kujitokeza kwa ujasiri. Katika hali nyingi, kwa msaada wa wananchi waliowasapoti, waliweza kuwazuia maadui na kuwashinda. Hakuna mtu mwingine aliyekuwa na ujasiri wa hata kusema jambo lolote, au hata kuelewa uzito wa tatizo hilo ipasavyo. Ni baada ya maulamaa kupaza sauti ndipo wengine walianza kufuata na kutoa sauti zao pia.

Kisrawi, ambaye anajulikana kuwa miongoni mwa wapinzani wakubwa wa maulamaa wa dini, alikiri kwamba mwanzo wa harakati ya katiba (mashruteh) ulitokana na ushirikiano wa busara kati ya Sayyid Behbahani na Sayyid Tabatabai. Ndiyo, katika siku hizo ambapo udikteta ulikuwa umejikita sana nchini Iran, hakuna mtu mwingine isipokuwa viongozi wa kidini aliyethubutu kusema chochote.

Mikataba ya aibu katika kipindi hicho ilifutwa kwa sababu ya upinzani na juhudi za maulamaa wa dini:

  • Mkataba wa Reuter ulizuiwa na Haji Mullah Ali Kani, Mwanazuoni mkubwa wa Tehran.
  • Mkataba wa tumbaku ulitenguliwa kwa fatwa ya Mirzā Shirāzī, kiongozi mkuu wa kidini, kwa kushirikiana na wanazuoni wakuu wa Iran.
  • Mkataba wa Vosough al-Dowleh ulifichuliwa na Modarres.
  • Harakati dhidi ya bidhaa za nguo za kigeni ilianzishwa na Agha Najafi Isfahani, kwa ushirikiano wa wanazuoni wa Isfahan na msaada wa wanazuoni wa Najaf.

Katika miaka ileile ambayo hawza ya Qom ilikuwa inaanzishwa, maeneo ya Iraq na mipaka ya Iran, hasa kwa uongozi wa Najaf na Kufa, yalishuhudia vita vya silaha kati ya wanazuoni na majeshi ya Uingereza. Si tu wanafunzi na walimu wa hawza, bali pia wanazuoni mashuhuri kama Sayyid Mustafa Kashani na watoto wa baadhi ya viongozi wa kidini walishiriki katika mapambano hayo; baadhi yao waliuawa shahidi na wengine walifukuzwa hadi maeneo ya mbali ya makoloni ya Waingereza.

Shughuli za viongozi wa kidini kuhusu suala la Palestina pia ni miongoni mwa mafanikio ya kujivunia ya hawza—iwe ni mwanzoni mwa karne, wakati siasa ya kuhamasisha na kuandaa wanazi wa Kizayuni ilipoanza, au katika miaka ya 1930, wakati sehemu muhimu ya Palestina ilikabidhiwa rasmi kwa Wazayuni na serikali ya Kizayuni kutangazwa. Barua na matamko yao juu ya suala hili ni miongoni mwa nyaraka za kihistoria zenye thamani kubwa.

Nafasi isiyo na kifani ya hawza ya Qom, na kisha hawza nyingine nchini Iran, katika kuanzisha harakati ya Kiislamu, kusababisha mapinduzi, kuelewesha umma, na kuhamasisha watu kwa ujumla, ni mojawapo ya alama kubwa za utambulisho wa jihadi wa taasisi hizi za kidini. Wanafunzi wa hawza, wakiwa na akili angavu na uwezo wa kuzungumza kwa ufasaha, walikuwa miongoni mwa wa kwanza kuitikia mwito wa Imamu Mujahid kwa haraka, kwa umakini na kwa subira licha ya madhara, ili kueneza fikra za mapinduzi na kuwaelimisha watu.

Kwa kuelewa ukweli huu, ndiyo maana Imamu Khomeini (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) katika ujumbe wake mzito kwa hawza alieleza kuwa:

  • Wanafunzi wa dini na maulamaa ndio waliotangulia kutoa maisha yao katika kila mapinduzi ya Kiislamu na ya watu.
  • Kazi ya mashujaa waliouawa shahidi ni njia ya kuelewa hakika ya "tafaqquh" (kuelewa kwa undani dini).
  • Aliwaona wanazuoni kama vinara wa uwanja wa jihadi, walinzi wa taifa, na watetezi wa wanyonge.

Imamu aliweka tumaini lake kubwa juu ya wanafunzi wa dini waliokuwa na hamasa ya mapinduzi na harakati za kijamii, na akaonyesha masikitiko kwa wale waliokuwa wakijifungia tu kwenye vitabu na masomo bila kujali masuala muhimu ya kijamii. Katika ujumbe huo alikemea sana watu wa mtazamo mgumu (muta'assibin) na aliwaonya kuhusu hatari ya maadui kutumia upumbavu wao kuingilia hawza. Alionya pia kuhusu mbinu mpya za watu wanaouza dini kwa sababu ya maslahi yao binafsi.

Kwa mtazamo wake wa busara, Imamu alieleza kuwa mabeberu wa kimataifa wako macho wakisubiri nafasi ya kushambulia heshima na ushawishi wa maulamaa wa Kiislamu wenye uelewa wa siasa. Katika maandishi hayo yaliyojaa hekima na mapenzi kwa dini, wasiwasi wake mkubwa ulikuwa kwamba fikra ya kutenga dini na siasa, au kufanya dini ionekane haipaswi kushughulikia masuala ya kijamii na kupinga dhulma, huenda ikachukua nafasi katika hawza na kuzuia maendeleo ya kweli.

Kudai kuwa dini inapaswa kutoshiriki katika siasa ni udanganyifu mkubwa ambao unawafaidisha sana wakoloni na maadui wa Uislamu, ambao kila mara wamepata hasara kutokana na kuingilia kwa wanazuoni wa kweli katika uwanja wa mapambano.

Utakatifu wa dini huonekana zaidi katika nyanja za jihadi ya kifikra, kisiasa, na hata kijeshi—na unaimarishwa kupitia kujitolea kwa wanazuoni na damu ya mashujaa wa dini. Mfano bora ni Mtume Muhammad (SAW), ambaye alipowasili Yathrib (Madina), alianzisha serikali ya Kiislamu, akaunda jeshi, na kuunganisha ibada na siasa katika msikiti mmoja.

Kwa hiyo, hawza ya kielimu lazima isimame pamoja na jamii na isijitenge na masuala muhimu ya watu, na ichukulie jihadi katika aina zake zote kama wajibu wa kidini inapohitajika.

Hii ndiyo kauli muhimu ambayo Imamu alisisitiza mara nyingi kwa wanazuoni wakubwa, walimu, na hasa kwa wanafunzi vijana wa hawza.

 Sehemu ya Nne – Kitovu cha Ushiriki katika Uundaji na Ufafanuzi wa Mifumo ya Kijamii

Nchi na jamii za kibinadamu huendeshwa katika nyanja zote za maisha ya kijamii kwa kutumia mifumo maalum ya kijamii. Hii inajumuisha:

  • Aina ya serikali na utawala (kama vile udikteta, mashauriano, n.k.),
  • Mfumo wa mahakama na utatuzi wa migogoro, makosa ya jinai na madai ya haki,
  • Mfumo wa kiuchumi na kifedha, masuala ya sarafu na fedha,
  • Mfumo wa kiutawala (uongozi wa ndani),
  • Mfumo wa biashara na kazi,
  • Mfumo wa familia, na mengine mengi.

Mambo haya yote ni sehemu ya masuala ya kijamii ya kila taifa, na katika jamii mbalimbali duniani, huendeshwa kwa njia tofauti na kwa kutumia mifumo tofauti.

Bila shaka, kila mfumo kati ya hiyo hujengwa juu ya msingi wa fikra fulani — iwe umetokana na mawazo ya wasomi na wataalamu, au umetokana na mila, desturi, na urithi wa jadi wa jamii husika.

 Katika serikali ya Kiislamu, msingi na kanuni za mfumo wa jamii lazima zichukuliwe kutoka katika Uislamu na maandiko yake sahihi. Mifumo ya kuendesha jamii inapaswa kutolewa kutoka katika mafundisho hayo.

Ingawa fiqhi ya Kishia, isipokuwa katika baadhi ya maeneo kama vile masuala ya mahakama, haijashughulikia vya kutosha uundaji wa mifumo ya kijamii, lakini kwa baraka ya kanuni pana za fiqhi zilizopatikana kutoka Kitabu (Qur’an) na Sunna, pamoja na msaada wa kanuni za sekondari (a’naawīn al-thāniyya), ina uwezo wa kutosha wa kubuni mifumo mbalimbali ya kuendesha jamii.

Katika suala la asili na chanzo cha utawala, kazi kubwa ya Imam Khomeini kuhusu Wilāyat al-Faqīh wakati wa uhamisho wake Najaf, ilikuwa ni mwanzo wa baraka uliofungua njia ya utafiti kwa wanavyuoni wa hawza. Baada ya kuundwa kwa Jamhuri ya Kiislamu, vipengele vyake mbalimbali vilikua katika nadharia na vitendo. Hata hivyo, bado katika mifumo mingi ya kijamii ya nchi, kazi hiyo haijakamilika na haijaratibiwa vizuri. Hawza ya kielimu inapaswa kuziba pengo hili, kwani hili ni miongoni mwa majukumu yake yasiyoepukika.

Leo, kwa kuwa mfumo wa Kiislamu umethibitika na umeanzishwa, jukumu la mwanazuoni wa fiqhi ni zito. Hatuwezi tena, kama asemavyo Imam Khomeini, kuichukulia fiqhi kama watu wasiojua wanavyochukulia—kuwa ni kuzama tu katika hukumu za mtu binafsi na ibada. Fiqhi inayojenga umma haipaswi kuishia tu kwenye hukumu za ibada au wajibu wa mtu mmoja mmoja.

Bila shaka, ili kubuni na kupanga mifumo ya kijamii, hawza inahitaji kufahamu kwa kiwango cha kutosha maarifa ya kisasa ya dunia kuhusu mifumo hiyo. Uelewa huu utamwezesha faqihi kutumia kwa busara yale yaliyo sahihi na yasiyo sahihi katika maarifa hayo, kisha kupitia Qur'an na Sunna, aweze kuchora muundo wa mifumo ya kijamii inayofaa kwa kuendesha jamii kwa mujibu wa fikra ya Kiislamu.

Mbali na hawza, pia vyuo vikuu vya nchi vina uwezo na pia jukumu katika jambo hili. Hili linaweza kuwa mojawapo ya maeneo ya ushirikiano kati ya hawza na chuo kikuu. Kazi kubwa ya chuo kikuu ni kufanya uhakiki na ukosoaji wa kielimu kuhusu maarifa yanayohusiana na sayansi za kijamii na mifumo ya utawala na maisha ya wananchi, kisha kwa kushirikiana na hawza, kuwasilisha maudhui ya fikra ya Kiislamu kwa njia inayofaa.

Sehemu ya Tano – Ubunifu wa Kimaendeleo katika Muktadha wa Ujumbe wa Uislamu kwa Dunia

Hili ni lengo kuu kabisa linalotegemewa kutoka kwa hawza (taasisi za elimu ya dini). Huenda baadhi wakaliona hili kuwa ni ndoto ya mbali au fikra ya kimajaliwa. Katika ile usiku ya kihistoria baada ya shambulio dhidi ya Madrasa ya Fayziyyah mwaka 1342 Hijria (sawa na 1963), wakati Imam Khomeini alipokuwa akizungumza na kundi dogo la wanafunzi waliokuwa wameshikwa na hofu, baada ya Sala ya Ishaa katika nyumba yake, alitamka maneno ya juu sana: “Hawa wataondoka, ninyi mtabaki.” Huenda kwa baadhi yetu wakati huo, haya yalionekana kuwa ndoto au maneno ya matumaini yasiyo na msingi. Lakini muda ulithibitisha kuwa imani, subira, na kutegemea Mwenyezi Mungu vinaweza kuondoa hata milima ya vizingiti, na njama za maadui haziwezi kushinda mapenzi ya Mwenyezi Mungu.

"Kusimamishwa kwa ustaarabu wa Kiislamu" ndilo lengo kuu la kidunia la Mapinduzi ya Kiislamu. Ustaarabu huu ni ule ambao ndani yake:

  • Sayansi na teknolojia,
  • Rasilimali watu na maliasili,
  • Nguvu ya kisiasa na kijeshi,
  • Na kila uwezo wa kibinadamu na maendeleo ya binadamu,

…vyote hutumiwa kwa ajili ya:

  • Haki ya kijamii,
  • Ustawi wa wote,
  • Kupunguza tofauti za kitabaka,
  • Kuendeleza hali ya kiroho,
  • Kuinua elimu,
  • Kuongeza maarifa ya kiasili,
  • Na kuimarisha imani ya kidini.

Ustaarabu wa Kiislamu umejengwa juu ya:

  • Tauhidi (umoja wa Mungu) na athari zake katika jamii na mtu binafsi,
  • Heshima ya binadamu kwa misingi ya utu wake—si kwa jinsia, rangi, lugha, kabila au jiografia,
  • Haki na utekelezaji wake katika nyanja mbalimbali,
  • Uhuru wa mwanadamu katika nyanja mbalimbali za maisha,
  • Na juhudi za pamoja katika kila uwanja unaohitaji mchango wa kijihadi.

Ustaarabu wa Kiislamu unakinzana kabisa na ustaarabu wa sasa wa kimaada. Ustaarabu wa kimaada ulianza na:

  • Ukoloni,
  • Kuteka ardhi za mataifa mengine,
  • Kudhalilisha mataifa dhaifu,
  • Mauaji ya halaiki ya watu wa asili,
  • Kutumia elimu kwa ajili ya kuwanyanyasa wengine,
  • Kudhulumu,
  • Kusema uongo,
  • Kulea matabaka ya kijamii yasiyolingana,
  • Na kueneza vitisho na ukandamizaji.

Kadri muda ulivyopita, ufisadi wa kimaadili na upotovu wa kijinsia vilianza kuingia katika ustaarabu huu na vikaendelea kukua.

Leo, mifano wazi na iliyokamilika ya ujenzi huu mbaya wa kimaendeleo tunayoiona katika nchi za Magharibi na wafuasi wao: kilele cha utajiri kilicho karibu na mabonde ya umaskini na njaa; unyanyasaji wa wale wanaopenda nguvu kwa kila mtu wanayeweza kumlazimisha; matumizi ya sayansi kwa mauaji ya kimbari; kuingiza ufisadi wa kijinsia ndani ya familia na hadi kwa watoto; udhalimu na ukatili usio na kifani katika mifano kama Gaza na Palestina; vitisho vya vita kwa sababu ya kuingilia mambo ya watu wengine, kama ilivyoonekana katika utawala wa Marekani katika nyakati za hivi karibuni.

Ni wazi kuwa ustaarabu huu wa batili utaondoka na kufutwa; hili ni sheria ya lazima ya uumbaji: "Hakika batili ni lazima lipotee." (Qur'an, 17:81) "Na yale yaliyokithiri, yatapotea bure." (Qur'an, 13:17). Kazi yetu leo ni, kwanza, kusaidia kubatilisha batili hii na pili, kuandaa ustaarabu wa mbadala kwa mtazamo na utekelezaji kadri iwezekanavyo. Kudai kuwa "wengine hawakuweza, basi sisi pia hatuwezi" ni upotoshaji. Wengine walipopigania kwa imani, kwa mahesabu sahihi, na kwa uvumilivu, waliweza kushinda. Mfano dhahiri na wazi mbele yetu ni: Mapinduzi ya Kiislamu na Jamhuri ya Kiislamu.

Katika mapambano haya, kutakuwa na madhara, maumivu, na hasara ambazo zitahitaji kustahimiliwa. Hapo, ushindi utakuwa wa hakika. Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alitoka Makka usiku na kwa siri kutoka miongoni mwa waabudu sanamu, akaenda kwenye pango, lakini baada ya miaka minane aliingia Makka kwa shangwe na nguvu, akitakasa Kaaba kutoka kwa sanamu na kuondoa waabudu sanamu. Katika miaka hii minane, aliteseka mno na alimpoteza msaidizi kama Hamza, lakini alishinda.

Ulinzi wa miaka minane wa vita takatifu wa Iran dhidi ya muungano wa watawala wa kimataifa wa mabeberu na waongo pia ni mfano mwingine. Hawza kubwa na yenye ufanisi ya leo ya Qum, ambayo mwanzoni ilikuwa inakutana na changamoto nyingi, pia ni mfano mbele yetu; na mifano hii inaweza kupatikana kwa wingi.

Hawza ya Sayansi ya Kidini ina jukumu kubwa katika sehemu hii, na jukumu hili ni, kwanza kabisa, kuchora michoro kuu na ndogo ya ustaarabu mpya wa Kiislamu, na kisha kuufafanua, kueneza, na kuhamasisha utamaduni wake katika jamii. Hii ni moja ya mifano bora ya "Ujumbe Dhahiri" (بلاغ مبین).

Katika kuchora muundo wa ustaarabu wa Kiislamu, fiqhi kwa namna fulani, na sayansi ya akili kwa namna nyingine, zote zina jukumu. Falsafa ya Kiislamu lazima iandike mwelekeo wa kijamii kwa masuala yake makuu. Fiqhi yetu pia, kwa kupanua mtazamo na ubunifu katika tafsiri, inapaswa kuainisha masuala mapya ya ustaarabu huu na kutoa hukumu zake.

Tamko wazi la Imam Khomeini kuhusu fiqhi na mbinu yake katika hawza ni mwanga. Katika tamko hili, mbinu ya tafsiri ni ile ya fiqhi ya jadi na kwa maneno yake yeye, "Ijtihad ya Jauhari"; ingawa, "wakati" na "maeneo" ni vipengele vinavyobainisha ijtihad. Inawezekana kwamba jambo lilikuwa na hukumu fulani katika wakati uliopita lakini kwa mabadiliko ya uhusiano wa kisiasa, kijamii, na kiuchumi, sasa linapata hukumu mpya. Mabadiliko haya ya hukumu hutokana na ukweli kwamba ingawa mada inaweza kuwa ile ile ya zamani, lakini kwa mabadiliko ya uhusiano wa kisiasa na kijamii, kimsingi imekuwa mada mpya, hivyo inahitaji hukumu mpya.

Zaidi ya hayo, matukio ya kimataifa na maendeleo ya kisayansi yanaweza kumfikisha faqihi mwenye ujuzi kwa ufahamu mpya kutokana na maandiko ya Qur'an na Sunnah, na kuwa sababu ya mabadiliko ya hukumu; kama ilivyokuwa mara nyingi katika mabadiliko ya maoni ya mujtahideen. Hata hivyo, fiqhi lazima ibaki kuwa fiqhi, na kutafsiri vibaya au kuharibu sheria za Kiislamu hakupaswi kutokea.

Kuhusu tafsiri na ufafanuzi wa jina la hawza ya sayansi ya dini na yaliyomo ndani yake, nitasema kwa kifupi, na sasa nitatoa maoni machache kuhusu hawza ya Qum ambayo sasa imefikia miaka mia moja.

Hawza ya Qom leo ni hawza hai na yenye maendeleo. Uwepo wa maelfu ya walimu, waandishi, watafiti, na wasomi katika maarifa ya Kiislamu, uzalishaji wa magazeti ya kisayansi na ya utafiti, pamoja na uandishi wa makala maalum na za jumla, kwa ujumla ni rasilimali kubwa kwa jamii ya leo na uwezo mkubwa kwa kesho ya nchi na umma. Kueneza masomo ya tafsiri, maadili, na kuongezeka kwa taasisi na masomo ya sayansi za akili ni nguvu muhimu ambayo hawza ya kabla ya mapinduzi haikuweza kuifikia.

Hawza ya Qom haijawahi kuwa na idadi hii kubwa ya wanafunzi na wasomi wenye mawazo. Uwepo wao katika maeneo yote ya mapinduzi na hata katika uwanja wa kijeshi na kutoa mashahidi wa thamani katika kipindi cha ulinzi wa kiakiolojia na kabla na baada yake, ni sifa kubwa ya hawza na ni sehemu ya mema yasiyo na idadi ya Imam Khomeini.

Kufungua njia ya ushawishi wa kimataifa na kuanzisha maelfu ya wanafunzi wa elimu kutoka kwa mataifa mbalimbali na uwepo wa wahitimu wake katika nchi nyingi ni kazi kubwa na isiyo ya kawaida ambayo inapaswa kutambuliwa. Uangalizi wa faqihi wa kisasa kuhusu masuala ya kisasa na masomo ya fiqh yanayohusiana nayo pia hutabiri mafanikio ya kisayansi na mageuzi ya kisayansi ya maendeleo. Kuongezeka kwa idadi ya wasomi vijana kwa uangalifu kuhusu masuala ya maarifa kutoka kwa maandiko ya Kiislamu yaliyohusiana, hasa Qur'an Tukufu, pia hutabiri kuwa Qur'an itapata umaarufu zaidi katika hawza ya kisayansi. Kuanzisha hawza za wanawake pia ni uvumbuzi muhimu na wenye athari kubwa ambao malipo yake ya milele yatakuwa kwa roho takatifu ya Imam Khomeini. Hawza ya Qom, kwa mtazamo huu, ni seti ya hai na inayoendelea na inamvua matumaini.

Hata hivyo, matarajio haya ya busara kwamba Hawza ya Qom iwe ya mbele na bora, bado inahitaji umbali mkubwa kutoka kwa hali ya sasa. Kutilia mkazo masuala yafuatayo kunaweza kupunguza umbali huu:

  • Hawza inapaswa kuwa ya kisasa; daima inapaswa kuendelea na wakati, na hata kwenda mbele ya wakati.
  • Kipaumbele kitatolewa kwa mafunzo ya nguvu katika sekta zote. Njia ya harakati ya taifa hili na mustakabali wa mapinduzi yatakuwa na nguvu kutoka kwa wale wataolewa katika hawza ya sayansi ya kidini.
  • Wana-hawza wanapaswa kuongeza uhusiano wao na watu. Mpango wa uwepo wa wasomi wa hawza kati ya watu na kuanzisha uhusiano mzuri na wao unapaswa kuandaliwa.
  • Wakuu wa hawza wanapaswa kwa busara kuzuia maoni mabaya ambayo yanaweza kumtia moyo mwanafunzi mchanga kuwa hana tumaini kuhusu mustakabali wake. Leo, Uislamu, Iran, na Shi’a katika ulimwengu vina heshima na hadhi ambayo havikuwahi kuwa nayo hapo awali. Mwanafunzi mchanga aendelee kusoma na kukua akiwa na hisia hii.
  • Kuangalia kwa matumaini kizazi kipya cha jamii na kujenga uhusiano nao kwa mtazamo huu. Sehemu muhimu ya vijana wa leo, waliotathmini akili, licha ya maoni mabaya yanayohusiana na hisia za kidini, bado wanadhihirisha imani kwa dini na wanaitetea, na wengi wao hawana uhasama na dini na mapinduzi. Kidogo sana cha watu wanakataa mwonekano wa kidini, hawapaswi kuchukua wazo hasi kuhusu hawza.
  • Mpango wa masomo ya hawza unapaswa kuandaliwa kwa njia ambayo fiqh inakuwa na ufanisi, inajibu masuala ya kisasa, na bila shaka ina imani, ina ujuzi wa kisasa, na inategemea mbinu ya ijtihad, ikiwa pamoja na falsafa inayojulikana na yenye mwelekeo wa kijamii na maoni yenye nguvu katika muktadha wa maisha ya jamii, na ikiambatana na maadili yenye nguvu ya imani na mawasiliano.
  • Zuhd, taqwa, kuridhika, kujitosheleza kwa Mungu peke yake, kutegemea Mwenyezi Mungu, roho ya maendeleo, na maandalizi ya kufanya mapambano yalikuwa na mashauri ya kila wakati kutoka kwa Imam Khomeini na wasomi wakubwa wa maadili na maarifa kwa wanafunzi wa hawza wa vijana, na sasa ninyi vijana wa hawza mnapaswa kuwa wapokeaji wa mashauri haya.
  • Kuhusu vyeti vya elimu vya hawza, pendekezo langu la kudumu ni kwamba cheti kiwe kilichotolewa na hawza yenyewe, na si taasisi yoyote ya nje. Ingawa, viwango vya daraja la elimu vya hawza vinaweza kutolewa kwa majina maarufu katika vyuo vikuu vya kitaifa na kimataifa, kama vile Shahada ya Bachelor, Shahada ya Uzamili, Shahada ya Utafiti (PhD), n.k.

Nitaishia hapa katika hotuba yangu kwa kusema maneno haya: Ninaomba kwa Mwenyezi Mungu kuongezeka hadhi ya Uislamu, nguvu na uthabiti wa umma wa Kiislamu, maendeleo na furaha ya Taifa la Iran, na ukuaji na ufanisi wa Hawza za Sayansi ya Dini, pamoja na ushindi dhidi ya maadui wanaotutakia mabaya, maadui wa nje, na wale wakaidi wa[ingaji wa ndani.

Salamu za Mungu ziwe juu ya Baqiyyatullah (roho zetu ziwe fidia kwa ajili yake na Mwenyezi Mungu aharakishe ujio wa faraja yake), na salamu za dhati ziwe juu ya roho za Mashahidi na roho tukufu ya Imam wa Umma.

Wasalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Ayatollah Khamenei: Jukumu la (Hawza) Chuo cha Kidini ni Kuchora Mipaka Mikuu na Midogo ya Ustaarabu mpya wa Kiislamu Sayyid Ali Khamenei

                           07 / 05 / 2025

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha